NYAMA kwa kawaida ni aina mojawapo ya chakula kitamu sana kwa binadamu,
tukila inatupatia virutubisho vingi vikihusisha protini, vitamini na
madini. Lakini kula nyama yoyote siyo tatizo wala shida kwa binadamu,
tatizo ni jinsi gani nyama hiyo inavyotayarishwa katika kupikwa,
kuchomwa na kuokwa ili mpaka binadamu apate kuila.
Tunapokula nyama huwa tunakula seli za misuli, na seli hizi za
misuli zinapokuwa nyingi na zimejirundika sehemu moja kwa wingi ndivyo
sehemu ya nyama hiyo inavyokuwa ngumu sana.
Kitendo cha kuipika
nyama ili ipate radha na tuweze kuila, kinaibadilisha nyama hiyo kwa
seli zake kuwa ngumu. Mabadiliko hayo makubwa yanayotokea kwenye
virutubisho vya protini, kuondosha majimaji na damu na hivyo seli za
nyama kushikamana.
Nyama inapochemshwa kwenye jotoridi la kati ya
600 C na 650 C, majimaji hutoka, protini hubadilika, na seli
zinajikunyata na kujikunja na kuwa ngumu tofauti na nyama inapokuwa bado
ni mbichi.
Kuchemsha nyama kwa joto kali kunafanya mabadiliko
kwenye nyama hasa ya kemikali aina ya amino. Virutubisho vya protini
ambavyo huchanganyika na kemikali ya kretani ambayo inakuwa kwenye seli
za misuli ya nyama na yenyewe hutengeneza kemikali nyingi aina za amino.
Kemikali hizi hutengenezwa kwa kiasi zikilinganishwa na uwiano wake
kwa kila gramu moja ya nyama.
Matokeo ya utafiti wa maabara na
majaribio ya kisayansi kwa wanyama yameonyesha kuwa kemikali hizi za
amino zitokanazo na nyama ni vianzilishi vikuu vya ugonjwa wa saratani
kwa binadamu.
Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani-
International Agency for Research on Cancer, limethibitisha kuwa
kemikali hizo za amino ni chanzo cha kusababisha ugonjwa wa saratani kwa
walaji wakuu wa nyama.
Utafiti huo umezidi kusisitiza na
kuonyesha kuwa walaji wa nyama wa kila mara wanajiweka katika hatari ya
kupatwa na ugonjwa wa saratani ya matiti na figo. Utafiti mwingine
uliofanyika mwaka jana, na Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani,
ulibainisha ya kwamba walaji wakubwa wa nyama ya ng’ombe, kondoo, mbuzi,
na nguruwe, wako katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa saratani ya
matiti hasa wanawake.
Watafiti wanayo maelezo mengi ya kwa nini
nyama imekuwa ni chanzo cha kusababisha ugonjwa wa saratani, Lakini
wanasisitiza kuwa kemikali za amino zinazopatikana kwenye nyama ndicho
chanzo kikuu cha kusababisha ugonjwa huo.
Katika maelezo yao
wanafafanua kwamba aina yoyote ya virutubisho vya protini, vikichomwa au
kuchemshwa, vinazalisha kemikali aina za amino, lakini kiwango cha
kemikali ya sumu katika mayai na maharage ya soya ni kidogo sana
ikilinganishwa na kiwango kinachopatikana kwenye nyama inapochomwa au
kuchemshwa.
Kiwango cha joto kinachotumika katika
kutayarisha nyama ili ipate kuliwa, ndicho hasa chanzo kikuu cha
utengenezwaji wa kemikali za amino kwenye nyama hiyo. Hivyo kuoka ,
kukaanga na kuchoma nyama, ni tatizo linalozalisha kemikali kwa vile
huhusisha matumizi ya joto kali.
Kemikali za amino huenea kwenye
milimita chache za mzunguko wote wa kipande cha nyama kufuatana na hali
ya nyama hiyo ilivyochomwa, kukaangwa au kuokwa.
Nyama ya kuchoma
ndiyo yenye madhara makubwa zaidi, kutokana na vile nyama hiyo
inapochomwa kufukizwa na moshi (polycyclic aromatic hydrocarbons), moshi
wenye kemikali zenye vichocheo vya kusababisha ugonjwa wa saratani.
Hizi kemikali zinatokana na moshi wa mkaa na wa mafuta yanayochuruzika
kutoka kwenye nyama inayochomwa.
Muda unaotumiwa katika
kutayarisha nyama nao unachangia katika kuzalisha kemikali za
kusababisha saratani kutoka kwenye nyama. Majaribio yaliyofanywa na
maabara kuu ya Lawrence Livermore National Labaratory, ya nchini
Marekani, yalionyesha kuwa nyama iliyokaangwa kwa muda wa dakika 10
kwenye mafuta ya jotoridi 2300C, ilikuwa na kiasi kingi cha kemikali
mara mbili zaidi ya nyama ya aina ile iliyokaangwa kwa jotoridi lilile
lakini kwa muda mfupi wa dakika 4.
Hivyo nyama ya kuku na samaki
inayookwa kwa muda mfupi na kuiva, ina madhara kidogo sana kwa afya ya
binadamu, kuliko ile ya kondoo nguruwe na ng’ombe inayotumia muda zaidi
kuokwa wakati wa kutayarishwa. Na nyama inayookwa kwenye jiko la kuoka
ina madhara zaidi ya ile inayochomwa na ya kukaangwa. Hii imethibitishwa
na watafiti kwa kukuta kiasi cha kemikali za madhara kwenye rojo
inayochuruzika kutoka kwenye nyama iliyookwa.
Wanasayansi pia
wanashauri matumizi ya viungo vya kulainisha nyama kabla ya kutayarishwa
kwa kupikwa, kuchomwa na kuokwa. Baadhi ya viungo vinavyopendekezwa
vina uwezo mkubwa wa kupunguza kemikali kwenye nyama inapotayarishwa.
Kiungo
aina ya vitunguu swaumu, vimethibitishwa na wanasayansi kupunguza sana
madhara ya kemikali za sumu kwenye nyama inapotayarishwa. Pia matumuzi
ya mafuta ya zeituni kwenye vyakula na kwenye kutayarisha nyama
kunapunguza sana hatari ya kupatwa na saratani ya utumbo mkubwa
inayotokana na kula nyama ya kukaanga.
Nchini Marekani, tishio la
kemikali zitokanazo na ulaji wa nyama kuwa ni chanzo cha ugonjwa wa
saratani, lilifahamika miaka 13 iliyopita. Utafiti uliofanyika
ulionyesha kuwa wanawake waliokuwa wanapendelea kula hambaga, nyama
choma ya ng’ombe na nguruwe, vilivyotayarishwa kwa dakika nyingi,
walikabiliwa na hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa saratani ya matiti kwa
mara nne zaidi ya wanawake wale ambao hawakutumia vyakula hivyo au
walivitumia kwa uchache.
Utafiti mwingine wa mwaka 2003,
ulionyesha ya kwamba madhara ya ugonjwa wa saratani ya utumbo mkubwa,
yaliongezeka maradufu kwa walaji wa nyama choma ya ng’ombe, iliyochomwa
kwa dakika nyingi nchini Marekani. Baada ya tatizo hilo kuelezwa na
kuifahamisha jamii, National Cancer Institute kwa sasa imetoa ripoti na
kueleza kuwa nyama choma ni chanzo cha ugonjwa wa saratani ya utumbo
mkubwa kwa asilimia 20. Wametahadharisha kuwa ugonjwa huo ni kwa walaji
wakuu wa nyama choma inayochomwa kwa muda mrefu, kwa wale ambao kwa
nadra wanakula kababu, hambaga na nyama choma, hawa hawana nafasi ya
kupatwa na madhara.
Pale ambapo viungo vya kulainisha nyama kama
haviwezi kupatikana kwa urahisi, na vikatumika kupunguza kemikali za
amino, ushauri ni kutumia njia zinazoshauriwa na National Cancer
Institute kama wanavyoelekeza.
Inaelekezwa kupika nyama kwa
jotoridi kidogo kwa muda mfupi . Kukatakata nyama ya kupika katika
vipande vidogo vidogo ambavyo vinaiva haraka kwa kutumia moto mdogo
ambao siyo mkali sana.
Kuchagua nyama ya kuchoma ambayo haina
mafuta, nyama ambayo ikichomwa haitatoa mafuta ya kudondokea kwenye
mkaa na kuungua na hivyo kuifukiza nyama inayochomwa kwa moshi wenye
kemikali zenye madhara ya kusababisha saratani.
Kupika nyama
kwanza kwenye jiko la Microwave kwa muda wa dakika mbili, kitendo
ambacho kinapunguza kwa wingi kemikali za amino kwa asilimia 90. Muda
wa kuichemsha nyama hiyo usizidi dakika mbili, na hivyo kusababisha
kuikausha nyama.
Kupasha nyama joto kabla haijapikwa, nyama
ifungwe vizuri na kuwekwa kwenye maji moto ambamo itakaa kwa muda wa
dakika 30 hadi 60. Nyama ikiondolewa kwenye maji moto, mara moja ipikwe
maana ni kawaida ya vimelea na bakteria kuzaliana haraka kwenye nyama
yenye joto.
Kugeuzageuza nyama mara kwa mara wakati wa kuchoma,
kunasaidia kupunguza upande mmoja wa kipande cha nyama kuchomwa na moto
na kuungua, wakati upande mwingine wa pili nyama bado ni mbichi. Nyama
huiva haraka kwa uwiano sawa na hivyo kutoruhusu kuzalishwa kwa kemikali
za sumu.
No comments:
Post a Comment