KITENDO cha binadamu kushindwa kutekeleza majukumu yake na kutumia
kilevi kama kichocheo cha nguvu za kutekeleza jambo hilo, ni dalili ya
ugonjwa wa akili.
Vile vile, imeelezwa kuwa, tabia ya watu wanaotumia ulevi wa aina
mbalimbali kukosa imani na kila mtu kwa kila jambo bila sababu za msingi
ni ugonjwa wa akili.
Mtaalamu
wa magonjwa hayo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi na Mkuu wa Sehemu
ya Magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Afya ya Akili na Dawa za Kulevya wa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Joseph Mbatia alisema hayo Dar
es Salaam jana alipozungumza muda mfupi baada ya uzinduzi wa kampeni
ya kuhamasisha jamii kuepukana na ulevi wa pombe wa kupindukia.
Kampeni hiyo itakayoendeshwa na vituo 11 vya redio nchini, vipererushi,
magazeti na njia nyingine za mawasiliano ya umma ilizinduliwa rasmi na
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni na zitadumu kwa miezi sita
ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu juu ya madhara ya pombe na
kubadili tabia ya ulevi.
Kwa mujibu wa Dk. Mbatia, idadi kubwa ya wagonjwa wa akili waliopo
nchini inatokana na ulevi wa kupindukia wa pombe na vileo vingine.
Katika hotuba yake ya uzinduzi, Nyoni alisema pombe ni hatari na
haipaswi kuendekezwa kwa kuwa inachochea umasikini kwa kiasi kikubwa,
ugomvi katika familia, kusambaa kwa maambukizi ya magonjwa ya kuambukiza
kama Ukimwi na madhara mengine mengi.
No comments:
Post a Comment