Mshituko wa moyo unatokea wakati
mtiririko wa damu yenye oksijeni unapozuiwa kwa ghafla katika misuli ya
moyo. Iwapo mzunguko huo wa damu hautoendelea haraka, kitendo hicho
huifanya misuli ya moyo kuharibika kwa kukosa oksijeni na hivyo
kuhatarisha maisha ya muathirika. Mshituko wa moyo kwa lugha ya tiba
unajulikana kama 'Myocardial Infarction' inayomaanisha "Myo".. muscles
au msuli, 'cardio'.... Heart au moyo na "infarct"....kufa kwa tishu
kutokana na kukosa oksijeni. Kama vilivyo viungo vingine mwilini hasa
misuli, moyo nao huhitajia damu. Bila damu seli za moyo hudhoofika suala
ambalo hupelekea mtu kuhisi maumivu. Mshituko wa moyo hutokea pale
mshipa mmoja wa damu au zaidi inaposhindwa kusafirisha damu yenye
oksijeni katika moyo, kutokana na kuziba mishipa hiyo. Mishipa ya damu
inaweza kuziba kwa sababu tofauti kama vile, kuta za mishipa ya damu
inayopeleka damu kwenye moyo (coronary arteries) kuwa nene, chembechembe
za mafuta kujikusanya katika mishipa ya damu, kudhoofika na kukonda
mishipa ya damu, mishipa ya damu inaposinjaa na kushikana au spasm na
kujitokeza donge la damu katika mishipa ya damu.
Mshituko wa moyo mara nyingi
husababishwa na ugonjwa wa moyo wa mishipa ya damu au Coronary Heart
Disease (CHD). Hii ni hali ambayo ndani ya mishipa ya damu hutokea kitu
kiitwacho 'plaque' na kuzuia damu isiweze kupita katika mishipa ya damu,
ambayo ni matokeo ya muda mrefu. Lakini ni wakati gani mtu hukabiliwa
na hatari ya kupata mshituko wa moyo? Ni pale umri wa mtu unapoongezeka
na kuwa mzee, mtu anapokuwa na unene wa kupindukia, kuvuta sigara, kuwa
na shinikizo la damu au High Blood Pressure. Kuishi bila kuwa na
harakati na kutoushughulisha mwili. Mtu kuwa na kiwango cha juu cha
mafuta katika damu au High Blood Cholesterol. Kuwa na ugonjwa wa
kisukari na kuwa na msongo wa mawazo, wasiwasi na fikra nyingi. Mambo
mengine yanayochangia kupata mshituko wa moyo ni baadhi ya magonjwa ya
moyo, kufanyiwa operesheni ya moyo, kuwa na ndugu katika familia ambao
wana matatizo ya moyo na jinsia ya kiume. Tunaelezwa kuwa, uvutaji
sigara husababisha mshituko wa moyo unaotokana na kuziba mishipa ya damu
kwa asilimia 36, ambapo unene husababisha ugonjwa huo kwa asilimia 20.
Kukaa bila kujishughulisha au kufanya mazoezi husababisha mshituko wa
moyo kwa asilimia 7-12. Pia wanaume wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na
mshituko wa moyo zaidi kuliko wanawake katika kipindi chote cha maisha
hasa kabla ya wanawake hawajafikia wakati wa kukatika hedhi. Lakini kwa
ujumla kwa kuwa wanawake huishi miaka mingi kuliko wanaume, magonjwa
mengine ya moyo husababisha vifo vya wanawake uzeeni zaidi kuliko
wanaume.