WELCOME

"Experience is not what happens to you; it is what you do with what happens to you." and "When you feel like giving up, remember why you held on for so long in the first place"Instead of giving myself reasons why I can't, I give myself reasons why I can." because always "When one door closes another door opens; but we so often look so long and so regretfully upon the closed door, that we do not see the ones which open for us."by ISI H


Monday, April 28, 2014

MSHTUKO WA MOYO NI NINI?

Mshituko wa moyo unatokea wakati mtiririko wa damu yenye oksijeni unapozuiwa kwa ghafla katika misuli ya moyo. Iwapo mzunguko huo wa damu hautoendelea haraka, kitendo hicho huifanya misuli ya moyo kuharibika kwa kukosa oksijeni na hivyo kuhatarisha maisha ya muathirika. Mshituko wa moyo kwa lugha ya tiba unajulikana kama 'Myocardial Infarction' inayomaanisha "Myo".. muscles au msuli, 'cardio'.... Heart au moyo na "infarct"....kufa kwa tishu kutokana na kukosa oksijeni. Kama vilivyo viungo vingine mwilini hasa misuli, moyo nao huhitajia damu. Bila damu seli za moyo hudhoofika suala ambalo hupelekea mtu kuhisi maumivu. Mshituko wa moyo hutokea pale mshipa mmoja wa damu au zaidi inaposhindwa kusafirisha damu yenye oksijeni katika moyo, kutokana na kuziba mishipa hiyo. Mishipa ya damu inaweza kuziba kwa sababu tofauti kama vile, kuta za mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo (coronary arteries) kuwa nene, chembechembe za mafuta kujikusanya katika mishipa ya damu, kudhoofika na kukonda mishipa ya damu, mishipa ya damu inaposinjaa na kushikana au spasm na kujitokeza donge la damu katika mishipa ya damu.



                                                          
Mshituko wa moyo mara nyingi husababishwa na ugonjwa wa moyo wa mishipa ya damu au Coronary Heart Disease (CHD). Hii ni hali ambayo ndani ya mishipa ya damu hutokea kitu kiitwacho 'plaque' na kuzuia damu isiweze kupita katika mishipa ya damu, ambayo ni matokeo ya muda mrefu. Lakini ni wakati gani mtu hukabiliwa na hatari ya kupata mshituko wa moyo? Ni pale umri wa mtu unapoongezeka na kuwa mzee, mtu anapokuwa na unene wa kupindukia, kuvuta sigara,  kuwa na shinikizo la damu au High Blood Pressure. Kuishi bila kuwa na harakati na kutoushughulisha mwili. Mtu kuwa na kiwango cha juu cha mafuta katika damu au High Blood Cholesterol. Kuwa na ugonjwa wa kisukari na kuwa na msongo wa mawazo, wasiwasi na fikra nyingi. Mambo mengine yanayochangia kupata mshituko wa moyo ni baadhi ya magonjwa ya moyo, kufanyiwa operesheni ya moyo, kuwa na ndugu katika familia ambao wana matatizo ya moyo na jinsia ya kiume. Tunaelezwa kuwa, uvutaji sigara husababisha mshituko wa moyo unaotokana na kuziba mishipa ya damu kwa asilimia 36, ambapo unene husababisha ugonjwa huo kwa asilimia 20. Kukaa bila kujishughulisha au kufanya mazoezi husababisha mshituko wa moyo kwa asilimia 7-12. Pia wanaume wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo zaidi kuliko wanawake katika kipindi chote cha maisha hasa kabla ya wanawake hawajafikia wakati wa kukatika hedhi. Lakini kwa ujumla kwa kuwa wanawake huishi miaka mingi kuliko wanaume, magonjwa mengine ya moyo husababisha vifo vya wanawake uzeeni zaidi kuliko wanaume.


Baadhi ya wakati mshituko wa moyo hutokea kwa dalili zilizo wazi na kwa haraka sana. Lakini mara nyingi mshituko wa moyo hutokea polepole huku mtu akipata maumivu ya wastani na kutokujisikia vyema. Mara nyingi watu wanaopatwa na hali kama hiyo huwa hawana uhakika na kile kinachotokea na husubiri kwa muda mrefu kabla ya kuomba msaada au kumuona daktari. Zifuatazo ni dalili ambazo hutokea pale mtu anapopatwa na mshituko wa moyo. 1) Maumivu katika kifua: Mara nyingi mtu anapopatwa na mshituko wa moyo huhisi maumivu sehemu za kifua hasa sehemu za katikati ya kifua ambayo huisha baada ya dakika kadhaa au mara nyingine maumivu hayo huisha na kurudi tena. Mtu huhisi kana kwamba kifua kinambana, kimejaa na kinauma. 2) Maumivu katika sehemu za juu za kiwiliwili: Mtu huhisi maumivu sehemu za mikono, mgongo, shingo, taya na tumbo. 3) Kukosa pumzi au kushindwa kupumua: Hali hii huweza kutokea ikichanganyika na maumivu ya kifua au bila maumivu hayo. Dalili nyinginezo ni pamoja na kutoka kijasho chembemba (cha baridi), kujisikia kichefuchefu pamoja na kichwa kuwa chepesi na kizunguzungu. Moyo kwenda mbio au kwa ibara nyingine mapigo ya moyo kutokea kwa kasi zaidi kuliko kawaida.
Unashauriwa iwapo utajisikia mumivu ya kifua, hasa pamoja na mchanganyiko wa moja ya dalili tulizozitaja, usisubiri na haraka mpigie simu daktari au wasiliana na kituo cha afya ili upatiwe msaada, au elekea haraka hospitali mwenyewe. Muda unaofaa wa kutibiwa mshituko wa moyo ni saa moja tangu wakati wa kutokea hali hiyo. Kutibiwa mapema dalili za mshituko wa moyo hupunguza hatari ya kuharibika seli za moyo. Hata kama huna uhakika dalili unazohisi ni za mshituko wa moyo au la, ni bora umuone daktari na ufanyiwe uchunguzi. Utafiti waliofanyiwa wanawake 515 ambao walipata mshituko wa moyo umeonyesha kuwa, wengi wao waliripotiwa kuwa na dalili za kujihisi kuchoka, kutolala vyema, kushindwa kupumua, kujisikia maumivu baada ya kula na wasiwasi. Asilimia 70 ya wanawake hao walihisi dalili zaidi ya moja kabla ya kupatwa na mshituko wa moyo.

Karibu theluthi moja ya kesi za ugonjwa wa mshtuko wa moyo hutokea kimya kimya, bila maumivu ya kifua wala dalili nyinginezo. Kesi kama hizo hugunduliwa baadaye katika vipimo. Kesi kama hizo hutokea zaidi kwa wazee, wagonjwa wa kisukari na baada ya kuunganishwa moyo au heart transplant. Wapenzi wasikilizaji tukisonga mbele na kipindi chetu sasa tuangalie vipimo vya mshituko wa moyo. Kwa kawaida madaktari hufahamu kuwa mtu amepatwa na mshituko wa moyo au anaelekea kupatwa na mshituko huo kutokana na dalili alizonazo na anavyojisikia. Pia kwa kutegemea historia ya kifamilia na ya kitiba ya mgonjwa pamoja na vipimo. Kipimo kikuu kinachotumika kupima iwapo mtu amepatwa na mshituko wa moyo ni EKG. Hicho ni kipimo kinachoonyesha na kurekodi mwendo na harakati ya moyo. Kipimo hicho huonesha moyo unakwenda kwa kasi ya kiasi gani, mapigo ya moyo na mdundo wake. Kwa hakika kipimo cha EKG huonyesha dalili za kuharibika moyo kutokana na matatizo ya mishipa ya moyo ya ugonjwa wa coronary heart disease na pia dalili za mshituko wa moyo uliotokea huko nyuma na unaotokea hivi sasa. Kipimo kingine ni cha damu ambacho huonesha protini zinazoonekana kwenye damu zinazotokana na seli za misuli za moyo zilizokufa. Wasikilizaji wapenzi kwa kuwa muda wa kipindi chetu unaelekea ukingoni, kwa leo hatutozungumzia namna ya kutibu na kuzuia ugonjwa wa moyo bali tutaangalia utafiti uliosema kwamba mshituko wa moyo mara nyingi hutokea saa tatu asubuhi. Wataalamu wa magonjwa ya moyo wamesema kuwa hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo hutokea zaidi mapema asubuhi, hasa saa tatu asubuhi.
Utafiti huo uliotangazwa katika Kongress ya 4 ya magonjwa ya moyo ya Mashariki ya Kati umeonyesha kuwa, watu wanaokabiliwa na hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo, hutokewa na ugonjwa huo mapema asubuhi kwa sababu ya mabadiliko ya homoni, ambayo huongeza hitajio la oksijeni la mishipa ya moyo katika wakati huo, na kusababisha mshituko wa moyo. Uchunguzi huo umeeleza pia kuwa, ripoti zinaonyesha ongezeko la matukio ya mshituko wa moyo katika siku za Jumatatu, suala ambalo huenda likawa linachangiwa na kiasi kikubwa na kula kupita kiasi siku za wikiendi. Wataalamu hao pia wamesema kuwa, mishipa ya juu ya mwili huwa inasinyaa msimu wa baridi, hali ambayo ni kinyume na utendaji wa mishipa ya moyo na husababisha kupungua kiwango cha oksijeni inayohitajiwa na misuli ya moyo. Wamesema hii ndio sababu, watu hupata mishtuko wa moyo kwa wingi wakati wa mapukutiko (fall) na baridi (winter).

No comments:

Post a Comment